UJUMBE WA KINABII KUHUSU
KUNYAKULIWA KWA KANISA

Kufuatia changamoto za kiimani ambazo jamii ya wanafunzi wa Yesu Kristo tunazipitia; na kutokana na matishio mbali mbali yanayotishia uhusiano wetu wa kiroho na Bwana Yesu; ni dhahiri kwamba umefika wakati wa kuzingatia vipaumbele vya imani ikiwa ni pamoja na kuzingatia ujumbe wa kinabii
kuhusu kunyakuliwa kwa kanisa la Kristo.

Mada hii inaanza kwa kuchambua maana ya misamiati wa kunyakuliwa, jinsi tukio litakavyokuwa, sababu za kunyakuliwa; na mchakato wa maandalizi ya unyakuo wenyewe. Karibuni.

MAANA YA KUNYAKULIWA

"Kunyakuliwa" ni tukio maalum la kinabii ambalo linatarajiwa kutokea wakati wowote kwa ajili ya kuhitimisha huduma za Kanisa la Kristo duniani. Tukio hili linawahusu makundi mawili ya walengwa. Kundi la kwanza ni kufufuliwa kwa wafu waliolala mauti katika Kristo! Na kundi la pili ni wanafunzi halisi wa Yesu Kristo tutakaokutwa hai. Na hii ni kwa mujibu wa maandiko ya Paulo alipowaandikia Wathesalonike:

"Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. Basi, farijianeni kwa maneno hayo." (1 THE. 4:13-18)

JINSI UNYAKUO UTAKAVYOFANYIKA

Tukio hili la kinabii litafanyika kwa kasi na kwa kushtukiza. Hakutakuwepo na taarifa ya kujiandaa kwa unyakuo. Maandiko yanasema kwamba itakuwa ni: "kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika." (1 KOR. 15:52)

Kwa sababu ya kushtukiza kwa tukio hili la ghafla imeandikwa ya kuwa kuna baadhi waliotakiwa kunyakuliwa wataachwa kwa sababu ni kwa ajili ya watakaokutwa wako tayari tu ndio watakaonyakuliwa:

"Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu." (MT. 24:37-42)

SABABU ZA KUNYAKULIWA

Baada ya kupitia tafsiri na jinsi unyakuo utakavyofanyika, napenda tupitie hoja muhimu za sababu za kunyakuliwa. Napenda kuzielezea sababu hizi kwa sababu kuna malumbano ya kitheolojia kuhusu unyakuo na mjadala ukilenga ni wakati gani unyakuo utafanyika.

Kuna kundi lenye kudai kunyakuliwa kutafanyika kabla kuanza kipindi cha miaka 7 ya dhidi kuu (Pre-tri-rapture) ; kundi la pili linaamini unyakuo utafanyika katikati ya kipindi cha miaka 7(Mid-tri-rapture); na kundi jingine linaamini kunyakuliwa kutafanyika mwishoni mwa dhiki kuu (Post-tri-rapture)

Uchunguzi wangu na imani yangu vinaangukia katika kundi la kwanza la(Pre-tri-rapture) na ndiyo maana nimeona nitoe sababu za kunyakuliwa kabla ya kuanza kipindi cha dhiki kuu.

1. Ahadi ya Yesu Kristo

Yesu mwenyewe ndiye aliyetangulia kuwajulisha wanafunzi wake kuhusu suala la kurudi tena kuwachukua ili wakae pamoja naye mbinguni: " Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo." (YN. 14:2-3)

2. Kuepushwa na ghadhabu ya Mungu

Mtume Paulo alidokeza habari za ujio wa Mpinga Kristo na atakavyotawala chini ya uvuvio wa Shetani mwenyewe. Na Kisha akataja habari za wale watakaochwa baada ya unyakuo watakavyoingia kwenye kipindi cha udanganyifu mkubwa wa Shetani kwa sababu walikataa kuamini kweli ya Injili kabla ya unyakuo:

Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake; yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo; na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa. Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo; ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu. (2 THE. 2:8-12)

Kwa hiyo, kunyakuliwa kabla ya kipindi cha utawala wa MpingaKristo ni ili tuepushwe na hii ghadhabu ya Mungu inayotarajiwa kuupata ulimwengu katika kipindi hicho: Kwa kuwa wao wenyewe wanatangaza habari zetu, jinsi kulivyokuwa kuingia kwetu kwenu; na jinsi mlivyomgeukia Mungu mkaziacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai, wa kweli; na kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye alimfufua katika wafu, naye ni Yesu, mwenye kutuokoa na ghadhabu itakayokuja. (1 THE. 1:9-10)

TISHIO LA KUACHWA KAMA HAKUNA MAANDALIZI

Kufuatia tukio la kunyakuliwa kufanyika ghafla, ndiyo maana maandiko yanahimiza walengwa wa unyakuo kuwa tayari wakati wote ili wasijekuachwa wakati wa unyakuo. Na hii ndiyo sababu ya kuamini kwamba unyakuo utafanyika kabla ya kipindi cha dhiki kuu ili walengwa wawe wametimiza vigezo vya unyakuo huo wasijepatwa na mabalaa ya dhiki kuu.

Ushahidi ni maandiko yanayo tahadharisha kuwa tayari, kutubu na kuishi maisha ya utakaso kamili wakati wote: "Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo." (UFU. 21:27)

Yesu mwenyewe aliyaonya makanisa ya Karne ya kwanza yajitakase na kujiweka tayari kwa unyakuo vinginevyo yatakosa fursa hiyo. Kwa Kanisa la Efeso alilionya akisema: "Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu." (UFU. 2:5)

Maana ya "Kuondolewa kinara" ni kufutiwa haki ya urithi wa ufalme wa mbinguni na kufutwa jina kwenye kitabu cha uzima. Mtume Paulo naye anasisitiza akisema kwa kuwa siku ya unyakuo yaja kama mwivi na itawakumba wote wasiojiandaa;akasema sisi tusikubali kubaki gizani mpaka tuvamiwe ghafla:

Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku. Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa. Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi. (1 THE. 5:2-4)

Tutaendelea na sehemu ya pili ambapo tutapitia mchakato wa maandalizi kwa ajili ya kunyakuliwa, ni mambo gani yatakayojiri baada ya unyakuo mbinguni na nini kitaendelea duniani. Tafadhali kama ujumbe huu umekugusa nijulishe kwa ku-like ukurasa huu na kisha warushie na marafiki zako wengine.

SEHEMU YA PILI
UJUMBE WA KINABII KUHUSU KUNYAKULIWA KWA MANISA

ZIJUE KAMBI ZA NADHARIA KUHUSU UNYAKUO

Kufuatia mwitiko na mrejesho wa makala hii sehemu ya kwanza, nimelazimika kuwasilisha uchambuzi na tathmini ya kambi za Nadharia kuhusu unyakuo ambazo kubwa ziko tatu. Moja inafundisha Unyakuo Kabla ya kipindi cha dhiki kuu (Pre.tribulation rapture); ya pili inafundisha Unyakuo utafanyika katikati ya Dhiki kuu (Mid-tribulation rapture), na ya tatu inafundisha Unyakuo utafanyika baada ya dhiki kuu (Post-tribulation rapture). Nitazitambulisha kwa kifupi na kutoa maoni yangu kwako msomaji wangu mpendwa:

KAMBI YA UNYAKUO KABLA YA DHIKI KUU

UNYAKUO KABLA (PRE-TRI) ni kambi ya nadharia inayofundisha ya kwamba kunyakuliwa kutafanyika KABLA ya kuanza kwa kipindi cha dhiki kuu. (Yh.14:1-4; 2 Thes.2:7-12).

Aidha, kambi hii inasimamia maandiko ya: "Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa. Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake..." (2 Thes.2:7-8)
Kambi hii inatetea msimamo wake kutokana na maneno ya Yesu aliyoliahidi kanisa la Thiatira kwamba ataliepusha lisiingie kwenye kipindi cha dhiki kuu (Ufu.3:10)

Kambi hii pia inayatafsiri maneno ya Yesu katika Injili ya Mathayo Sura ya 24 kuwa ni maonyo ya kinabii kwa ajili ya taifa la Israeli na majanga yatakayowapa wakati wa dhiki kuu na sio kwa kanisa

KAMBI YA UNYAKUO KATIKATI MWA DHIKI KUU

Kambi hii yenyewe imeamua kusimama katikati na kufundisha ya kuwa Kanisa lazima lipitie katika dhiki: (Matt. 5:11-12, 10:34-35, 24:1-31; Mk.13:1-27; Lk 21:1-28; Yh 16:33, 17:15; Yk1:2-15; 1 Pet. 4:12-19).

Kambi hii ya unyakuo kufanyika katikati mwa dhiki kuu ni utetezi kwamba Kanisa halitashiriki mapigo ya ghadhabu ya Mungu (Lk 21:36). Kwa hiyo Kanisa litanyakuliwa katikati ya dhiki kuu ili kuepushwa ghadhabu ya Mungu katika dhiki kuu ((Rum. 5:9; 1 Thes. 1:10, 5:9)

KAMBI YA UNYAKUO BAADA YA DHIKI KUU

Kambi hii ni kongwe na inafundisha ya kwamba Kanisa litakuwepo katika dhiki kuu na kunyakuliwa mwishoni mwa dhiki kuu ((Matt. 24:29-31)

Msimamo wa kambi hii unasimamia nukuu za maandiko yasemayo: Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe. Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu yeyote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo. (MT.24: 21-22)

Kisha wanasimamia nukuu za maneno ya Lakini mara , baada ya dhiki ya siku zile……..ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni……nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi…… Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu. (MT. 24:29-31)
Kisha wanatumia nukuu za maneno yasemayo:“…Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule. (MT. 24:24)

Kwa mtazamo wa kambi hii msamiati wa neno wateule unatafsiriwa kuwa ni kanisa! Wanafundisha ya kwamba: i) Kanisa litakuwepo duniani kwa kipindi chote cha dhiki ya siku za mwisho, ii) Kanisa litakutana na upinzani wa Mpingakristo na chapa yake ya mnyama, iii) Kila mtu duniani, wakiwemo wote wanaomwamini Yesu Kristo, watashinikizwa kufanya maamuzi ya kukubali au kukataa chapa ya mnyama, iv) Kanisa lazima lijiandae kwa nyakati ngumu zitakazolikabili kwenye dhiki kuu, v) Kanisa litanyakuliwa mwishoni mwa dhiki kuu

UCHAMBUZI WANGU KUHUSU KAMBI ZA UNYAKUO

Kwanza naomba nieleweke kwamba miye sio mshabiki wa kambi za nadharia kwa kufuata mkumbo. Nimefundishwa na kuzoezwa kufanya utafiti binafsi katika maandiko na kupata tafsiri na matumizi sahihi ya maandiko. Sasa inapotokea utafiti wangu ukaangukia kati ya moja wapo ya kambi husika, hiyo haina maana ya kwamba mimi ni mwana-kambi hiyo kwa ushabiki tu.

Kwa mujibu wa kambi za nadhari kuhusu unyakuo, utafiti wangu umejikuta ukiangukia kwenye kambi ya kwanza ambayo ni Unyakuo kabla ya kipindi cha dhiki kuu Nimezifuatilia hoja zao na tafsiri ya maandiko nikathibitisha ndivyo yalivyo.

Hata hivyo, ilinichukua muda mrefu kujifunza kwa umakini kuhusu hoja za kambi ya Unyakuo baada ya dhiki kuu (Post-tribulation rapture) ili kujua usahihi wa kile wanachoamini, chimbuko la kambi yenyewe na mwelekeo wake kiimani.

Katika utafiti wangu nilikuja kugundua eneo moja kubwa ambalo viongozi wa kambi hii walighafilika na kutoka nje ya tafsiri sahihi na hiyo ikazifanya hoja zao zote nazo kupoteza maana yake halisi.
Eneo hilo kutafsiri ya kwamba, kanisa litakuwepo kwenye dhiki kuu kwa vile limetajwa kwa jina la wateule kama tulivyosoma kwenye baadhi ya nukuu za maandiko.

Uchambuzi wangu katika eneo hilo ni kutumia maandiko hayo hayo kuthibitisha kwamba wateule wanaotajwa kwenye maandiko husika hayalihusu kanisa badala yake yanalihusu Israeli kama taifa. Na kama wateule ni Israeli na sio kanisa dhana nzima ya kunyakuliwa baada ya dhiki kuu inapoteza uhalali wake kimaandiko. Hoja zangu za utetezi ni kama ifuatavyo:

1. Mjadala wa mazungumo ulihusu taifa la Israeli

Katika Mathayo 24: Yesu alikuwa anajibu maswali ya wanafunzi wake kwa mtazamo wa Israeli kama taifa na sio kwa mtazamo wa kanisa. Ushahidi ya kwamba aliongea nao kwa mtazamo wa Israeli badala ya kanisa ni maneno yake ya: hapo mtakapoliona chukizo la uhabiribu.limesimama katika patakatifu……ndipo walio Uyahudi na wakimbilie milimani…” (MT.24:15-16)

2. Kipaumbele cha huduma ya Yesu kilikuwa ni Israeli

Yesu mwenyewe alikwisha kujitambulisha kwamba ujio wake na huduma yake kipaumbele chake kilikuwa ni kwa taifa la Israeli na sio mataifa: Akajibu, akasema, sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. (MT.15:24). Na sio kwamba kipaumbele chake ni kwa Israeli kama taifa tu, hata alipowatuma wanafunzi wake ambao wote walikuwa ni wayahudi hakuwapa ruhusa kutembelea watu wa mataifa: Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. (MT.10:5-6)

3. Katika Ufunuo, Kanisa halitajwi kabisa kwenye kipindi chote cha dhiki kuu

Katika sura tatu za kwanza za kitabu cha ufunuo, Kanisa limetajwa mara kumi na tisa lakini kuanzia Sura za 4-18 ambamo tunasoma taarifa za kina za kipindi cha miaka 7 ya dhiki kuu kanisa halitajwi humo hata mara moja.

Kana kwamba hii haitoshi, kwenye sura ya 3:10 tunakuta Yesu alikwisha kuliahidi kanisa ya kwamba ataliepusha lisiingie kwenye saa ya kujaribiwa kwa ulimwengu: Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi name nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi.

MWELEKEO WA UNYAKUO KABLA YA DHIKI

Unyakuo wa kanisa kabla ya kipindi cha dhiki kuu ndipo Yesu anapotimiza ahadi ya kuturithisha ufalme wa mbinguni na kuwa pamoja naye mbinguni (Yh.14:1-3) Kunyakuliwa kunajumisha: i) Waliokufa katika Kristo kufufuliwa (1 Thes.4:13-16), ii) Tuliosalia kuvalishwa miili mpya na kunyakuliwa mawinguni (1 Thes.4:17), iii) Kukutana kwenye Kiti cha hukumu cha Kristo kwa ajili ya thawabu mbinguni (2 Kor.5:10), iv) Kushikiri karamu ya arusi ya Mwanakondoo mbinguni (Mt.26:29; Ufu.19:7-9)

Bado mada inaendelea. Najua uchambuzi wangu umetibua sana mitazamo ya kambi ya nadharia za unyakuo. Mimi simo kwenye kambi hata moja ila ninasimamia tafsiri sahihi ya maandiko ambayo yamekuwepo kabla ya kambi za nadharia zilizopo.

Sehemu inayofuata nitaendelea kufafanua ni kwanini kambi ya unyakuo baada ya dhiki inasimamia kwamba wateule ni kanisa’’ na sio Israeli hata kama maandiko yenyewe wanayosimamia sivyo yasemavyo. Kama umeguswa na mada nisaidie kwa ku-like post hii na kisha uwarushie na marafiki zako. Ubarikiwe sana.

SEHEMU YA TATU
UJUMBE WA KINABII KUHUSU KUNYAKULIWA KWA MANISA

Kwenye sehemu ya pili ya mada hii nilisimulia habari za kambi za nadharia za unyakuo pamoja na imani yangu. Niliahidi katika sehemu ya kuchambua ni kwanini kambi ya unyakuo baada ya dhiki inasimamia kwamba wateule ni kanisa’’ na sio Israeli hata kama maandiko yenyewe wanayosimamia sivyo yasemavyo. Lakini kutokana na mrejesho niligundua kuwepo kwa utata wa kuchanganya matukio mawili tofauti kuwa tukio moja. Katika sehemu hii ya tatu nimeona nitoe ufafanuzi na kisha kudokeza kuhusu hatari ya mtazamo wa madai ya kanisa kuwepo kwenye dhiki kuu:

ZIJUE TOFAUTI KATI YA "KUNYAKULIWA
KANISA" NA "YESU KURUDI MARA YA PILI"

Unyakuo na kurudi mara ya pili ni matukio mawili tofauti japokuwa yote ni matukio ya siku za mwisho na yote yanamlenga Yesu mwenyewe. Kuna utata katika kupambanua baadhi ya maandiko kama yana maana ya unyakuo au Yesu kurudi mara ya pili dunia.

Tukio la Unyakuo ni wakati Yesu Kristo anakuja kulichukua kanisa kutoka duniani kwenda mbinguni kama ilivyoandikwa katika (1 Thes 4:13-18; 1 Kor. 15:50-54.) Waliokufa katika Kristo watafufuliwa na tulio hai tuliosalia tutabadilishwa miili na kunyakuliwa ili kumlaki Bwana mawinguni. Kwa maelezo mengi unyakuo unalenga kanisa tu. Lakini wakati wa Yesu kurudi mara ya pili duniani, walengwa ni taifa la Israeli na hukumu dhidi ya mataifa yatakuwepo duniani kwa wakati huo, kufuta uovu na kusimika utawala wa milenia duniani (Rev.19:11-16; )

1. Wakati wa unyakuo watakatifu (kanisa) tunakutana na Bwana mawinguni (1 Thes.4:17). Wakati Yesu anaporudi mara ya pili duniani anakuja pamoja na watakatifu wake (kanisa) (Ufu. 19:14).

2. Wakati tukio la unyakuo Litafanyika kabla ya dhiki kuu (1 Thes.5:9; Ufu. 3:10). Tukio la Yesu kurudi mara ya pili duniani litafanyika baada ya dhiki kuu (Ufu 6-19)

3. Tukio la unyakuo linafanyika kuwaepusha watakatifu (kanisa) na dhiki kuu (1 Thes. 4:13-17, 5:9). Wakati Yesu kurudi kwake mara ya pili duniani ni kwa ajili ya kuwaokoa wayahudi na kuyahukumu mataifa yote yaliyokuwa upande wa Mpingakristo (Mat.24:40-41).

4. Tukio la unyakuo litakuwa ghafla na siri (1 Kor. 15:50-54). Wakati Yesu atakaporudi mara ya pili duniani kila jicho litamwona (Ufu. 1:7; Mat. 24:29-30).

5. Kurudi kwa Yesu duniani mara ya pili ni tukio litakalofanyika baada ya matukio kadhaa yaliyotabiriwa kufanyika katika siku za mwisho (2 Thes. 2:4; Mat.24:15-30; Ufu. 618). Lakini unyakuo ni tukio linalotarajiwa kufanyika wakati wowote kuanzia hivi sasa (Tit.2:13; 1 Thes. 4:13-18; 1 Kor. 15:50-54).

HATARI YA KUAMINI KANISA
LITAKUWEPO DUNIANI WAKATI WA DHIKI

1. Madai ya kwamba kanisa litakuwepo duniani kwenye dhiki kuu yanakinzana na agizo la Yesu la kuhubiri Injili kwa kila kiumbe ili aaminiye na kubatizwa ataokoka na asiyeamini atahukumiwa (MK.16:16) Kwa maana katika kuamini injili mtu anapata ahadi ya uzima wa milele ambayo kilele chake ni kuingia mbinguni; na asiyeamini anakuwa chini ya hukumu ya milele kwenda jehanamu ya milele

2. Madai ya kwamba kanisa litakuwepo duniani kwenye dhiki kuu mpaka mwisho yanakinzana na Ahadi ya Yesu Kristo kwa wanafunzi wake kuwa kaenda kuwaandalia mahali mbinguni na kisha "atarudi tena kuwachukua" ili alipo yeye mbinguni na wao wawepo pamoja naye (YH.14:1-3;1 Thes.4:17).

3. Madai ya kwamba kanisa litakuwepo duniani kwenye dhiki kuu mpaka mwisho yabatilisha unabii kwa kanisa kukusanyika mbele ya Kiti cha hukumu cha Kristo kwa ajili ya kupokea thawabu na taji za utukufu kwa ajili ya utumishi wao katik Kristo walioufanya wakiwa hai duniani.( 2Kor.5:10)

4. Madai ya kwamba kanisa litakuwepo duniani wakati wote wa dhiki kuu yanamfanya Mungu akiuke neno lake la kutokuwahukumu wenyehaki na waovu pamoja. (1 Thes.1:10; Ufu.3:10) Dhiki kuu ni hukumu ya Mungu ya kuifanya Israeli imkubali Masihi waliyemkataa (Yer.30:7) na kisha kuyahukumu mataifa yaliyokubali chapa ya mpingakristo wakati wa dhiki kuu. (Mt.25:32-34)

5. Madai ya kwamba kanisa litakuwepo duniani wakati wa dhiki kuu kunadhoofisha imani ya kujikana nafsi na kuishi maisha ya utakatifu duniani. Maana faraja ni matumaini ya kuingia mbinguni; Kisha sisi tulio hai tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. Basi farijianeni kwa maneno hayo. (1 Thes.4:17-18)

Tukutane kwenye sehemu ya nne. Kama umeguswa na mada nisaidie kwa ku-like post hii na kisha uwarushie na marafiki zako. Ubarikiwe sana.

SEHEMU YA NNE
UJUMBE WA KINABII KUHUSU KUNYAKULIWA KWA MANISA

UFAFANUZI KUHUSU WATEULE KATIKA MATHAYO 24 NI AKINA NANI

Kambi za nadharia kuhusu unyakuo wa kanisa zina malumbano ya karne nyingi kuhusu tafsiri ya msamiati wa neno wateule waliotajwa na Yesu Kristo kwenye maandiko ya Injili ya Mathayo 24. Maandiko hayo kama ifuatavyo:

"Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo." (MT.24:22); "Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule." (MT. 24:24); "Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu." (MT.24:31; Isa 11:12)

Kwa mujibu wa kambi ya nadharia ya Kanisa litapitia dhiki kuu (Post-tribulation rapture) wao wanatafsiri kwamba wateule wanaotajwa katika dhiki kuu ni kanisa na sio Israeli. Kambi ya nadharia ya unyakuo kabla ya kipindi cha dhiki kuu (Pre-tribulation rapture) wanasema wateule wanaotajwa hapa ni Israeli na sio kanisa kwa kuwa litakuwa limekwisha kunyakuliwa kabla ya dhiki kuanza.

VIGEZO VYANGU VYA UCHAMBUZI

Kama nilivyokwisha kutoa msimamo wangu huko nyuma na hapa narudia tena kuthibitisha ya kwamba, mimi si mshabiki wa kambi za nadharia kwa sababu zote zimeibuka baada ya maandiko yanayobishaniwa yalikwisha kuwepo. Vigezo vya uchambuzi ninavyotumia vinazingatia ukweli wa mambo yafuatayo:

Kwanza, nachunguza ni wakati gani maneno yalioandikwa yalisemwa na ni katika mazingira gani ya wakati huo. Kwa sababu wakati maneno yaliposemwa sio kwamba ndio wakati huo huo yalipoandikwa! Kuna wakati tofauti kati ya "kusemwa maneno" na wakati "maneno hayo yalipoandikwa"!

Pili, nani walengwa wakuu wa maneno yaliyosemwa kwa wakati huo (wayahudi au mataifa?) Hapa pia nazingatia utamaduni wa lugha iliyotumika na jamii ya wakati huo (kiebrania, kiaramu au kiyunani, kilatini nk)

Mantiki ya kuzingatia lugha iliyotumika wakati maneno yaliyosemwa ni kwa sababu lugha iliyotumika kusema maneno husika sio lugha hiyo hiyo ndiyo iliyotumika katika kuyaandika maneno hayo!

Tatu, ni akina nani waliohusika kutafsiri maandiko kutoka lugha asilia iliyotumiwa na waandishi asilia kuja kwenye lugha nyingine! Mfano toka Kiebrania kuja Kilatini au Kiingereza; toka Kiyunani kuja Kiingereza. Pia ni wakati gani kazi ya kutafsiri ilifanyika na kwenye mazingira gani ya kihistoria.

Mwishoni kabisa ndio nakuja kwenye kuzichambua "kambi za shule za nadharia" kuanzia chimbuko la kila nadharia husika kihistoria na kiitikadi. Kwa hiyo utakapoona majibu yangu yakaangukia kwenye msimamo wa mojawapo ya kambi za nadharia nisihukumiwe kwamba miye ni mfuasi wa nadharia hiyo.

Na sasa naanza kutoa uchambuzi wangu kuhusu wateule waliotajwa kwenye Injili ya Mathayo 24 ni akina nani? Ni kanisa au Israeli?

WATEULE NI ISRAELI NA SIO KANISA

1. Yesu alitumwa kwanza kwa Israeli kabla ya Kanisa

Mwenye kunishawishi kwa 100% niamini kuwa wateule wanaotajwa kwenye MT 24 ni Israeli na sio kanisa ni maneno ya Yesu mwenyewe kama alivyojieleza kwenye Injili hiyo hiyo ya Mathayo. Yesu anawataja walengwa wake wakuu wakati wa kipindi chote cha huduma yake akisema: “……Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. (MT. 15:24)

Na hata wakati anawatuma wanafunzi wake kwenda kuhubiri kwa mara ya kwanza aliwapa masharti ya kutokwenda kwa mataifa mengine, wala kwa wasamaria: Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. (MT.10:5-6)
Kwa mantiki hii, ni dhahiri ya kwamba maneno ya Yesu aliyokuwa kwenye mistari inayotaja wateule walengwa wake ni Israeli na sio Kanisa

2. Dhiki iliyotajwa na Yesu katika Mathayo 24 inahusu Israeli na sio kwa kanisa

Kama nilivyothibitisha hapa juu ya kwamba walengwa wakuu wa Yesu ni Israeli na sio kanisa; majibu hayo yanaendelea hata kwenye kipengele cha walengwa wa dhiki kuu. Mjadala wenyewe unaanzia kwenye jengo la hekalu. Wanafunzi walipomwonyesha hekalu naye aliwajibu bila kumungunya maneno akisema:

..Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa. Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani; (MT. 24:2,15-16)

Maneno ya unabii wa Danieli yalitaja moja kwa moja kuwa dhiki italipata taifa la Israeli pamoja na mji wake Yerusalemu (Dan.9:24) Na Yesu mwenyewe anasisitiza kiunabii akisema ikiwafika dhiki walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani.

Na mahali pengine Yesu anasema kwa kuwahurumia: Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato. (MT.24:20)
Kwa kifupi, mazungumuzo kati ya Yesu na wanafunzi wake yenye misamiati ya maneno ya injili ya Ufalme (24:14), patakatifu (24:15, na sabato (24:20) yote hii inalenga taifa la Israeli na sio kanisa.

Nabii Yeremia yeye alifunuliwa na kuipa jina dhiki kuu hiyo kuwa ni taabu ya Yakobo: Ole! Maana siku ile ni kuu, hata hapana inayofanana nayo, maana ni wakati wa taabu yake Yakobo; lakini ataokolewa nayo. (YER.30:7)

KANISA HALIKUWEPO WAKATI HUO KWENYE MATHAYO 24

Madai ya kwamba wateule waliotajwa katika Mathayo 24 ni kanisa na sio Israeli ni dhana ya kufikirika bila ushahidi kamili.

Ifahamike ya kwamba, Yesu Kristo alikwisha kusema msamiati kuhusu kanisa kwenye Injili hiyo hiyo ya Mathayo. Alipowahoji wanafunzi wake wanamtambua kama nani na Petro akajibu kuwa ni Mwana wa Mungu Aliye Hai ndipo Yesu alitabiri habari za ujio wa kitu alichokiita kanisa: Nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.. (Mat.16:18).

Muktadha wa msamiati wa lugha kuhusu "kanisa" linalotajwa hapa unalilenga kitu kitakachokuwepo baadaye na sio kwamba ni kitu kilichokuwepo kwa wakati huo! Sehemu ya pili ambayo Yesu alitumia msamiati wa neno "kanisa" ni kuhusu mchakato wa kusamehe na kupatana utakaozingatia mara kanisa litakapokuwa limeanza hapo baadaye:

....na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikilzia kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru (Mat.18:17). Maneno haya yoye hayakulenga kuwepo kwa kanisa kwa wakati huo kwa sababu lilikuwa halijakuwepo bado. Yalikuwa ni maelekezo ya Yesu yatakayotumika baadaye.

Kama "wateule" waliotajwa kwenye Mathayo 24 wangelikuwa ni "kanisa" Yesu asingemung'unya maneno angelitaja moja kwa moja kuwa "wateule" hao ni "kanisa"! Lakini kama Yesu hakusema ni "kanisa" maana yake tafsiri ya "wateule" hao sio kanisa.

Kwa mantiki hii maneno mengi yaliyosemwa na Yesu walengwa wake wakuu walikuwa ni kwa Israeli ya Agano la kale na sio Agano Jipya, kwa sababu hata mazingira ya kihistoria ambamo Yesu alikuwa akihudumu yalikuwa ni katika kipindi cha Agano la Kale chini ya torati ya Musa na hekalu ibada za kiyahudi. Agano Jipya limeanza rasmi baada ya kusulubiwa msalabani kufa na kufufuka kwake. Kwa hiyo kabla ya kifo na kufufuka kwa Yesu kanisa halikuwepo.

Sehemu itakayofuata nitajibu kuhusu swali tata la watakatifu katika dhiki kuu ni akina na wanatokana na nini? Ni kanisa ambalo halijanyakuliwa au ni Israeli au ni jamii nyingine? Ikiwa mada hii imekubariki nijulishe kwa ku-like na warushie marafiki zako pia. Ubarikiwe sana.

SEHEMU YA MWISHO
UJUMBE WA KINABII KUHUSU KUNYAKULIWA KWA KANISA

UTANGULIZI

Nimesoma michango ya majibu ya wasomaji pamoja na maswali maswali mbali mbali yaliyoulizwa. Maswali yote yaliyoulizwa kwenye sehemu ya nne yameulizwa nje ya mada. Ninaheshimu michango yote iliyotolewa kwa sababu kila utu wa mtu ni mawazo yake na ustaarabu kuheshimu mawazo ya mtu.  Hata hivyo, maelezo yangu yote yalijikita katika kujibu kile ambacho Mathayo 24 iliandika kuhusu WATEULE kama ni KANISA au ISRAELI. Nilionesha maaelezo ya Yesu mwenyewe jinsi alivyosema kuwa alikuwa anaongea na taifa la Israeli na kwamba kanisa kwa muda huo lilikuwa halijakuwepo. Kwa yeyote asiyekubaliana na ukweli huu hilo ni suala la kimapokeo zaidi lakini si la tafsiri sahihi ya kibiblia.

Hii ni sehemu ya mwisho kuhusu mada hii. Yakiwepo maswali ynayolenga mfululizo wa mada hii tangu mwanzo ambayo msomaji anaona haijaeleweka nitakuwa tayari kujibu kwa kifupi kabla ya kufungua mada mpya. Vinginevyo nimesukumwa kuandika kitabu kinachohusu mada hii na kitakapokamilika msomaji wa ukurusa huu utakuwa wa kwanza kupata habari zake. Kwa sasa napenda kufunga mada hii kwa kuelezeka kwa mukhtasari tu kuhusu habari za DHIKI na mchakato wa mambo yakayojiri siku za mwisho:

TAFSIRI YA DHIKI KINABII

Taabu ya uchungu uliokithiri; mateso makali kupindukia; mazingira magumu yasiyovumilika. Dhiki ni kipindi ambacho ghadhabu ya Mungu itamwagwa juu ya ulimwengu uliomkataa Mungu kwa kipindi kirefu tangu alipomtuma Mwanawe Yesu Kristo kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Walimwengu walichagua uongo badala ya kweli na kuzidi katika uovu sugu kwa karne nyingi. Mungu alikuwa mvumulivu kwao kwa muda mrefu na sasa uvumilivu wake utafikia ukomo.

"Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe.  Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo." (MT. 24:21-22)

"Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo; na wakati huo watu wako wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile." (DAN.12:1)



KUSUDI LA DHIKI KUU

Kusudi kubwa la kipindi cha dhiki ni kuliandaa taifa l Israeli kumkubali Masihi ambaye walimkataa wakati alipokuja kwao kwa mara ya kwanza. Kama ilivyoandikwa ya kwamba: Alikuja kwa walio wake lakini hawakumpokea, bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu.(YH.1:11-12) Kwa Israeli kumkataa Masihi, fursa ya neema ikapelekwa kwa Mataifa mpaka mpaka muda wake utakapokamilika (Rum.11:25-27)

Kipindi cha dhiki kimetafsiriwa kiunabii kuwa ni wakati wa taabu ya Yakobo (Yer.30:7) kwa sababu ni wakati ambapo Mungu anashughulika na taifa la Israeli. Huu ndio wakati uamsho wa kiroho kwa wayahudi utasambaa kila kona ya dunia. Wengi watamwamini Yesu na kuanza kuandaa kizazi kipya cha Israeli watakaoingia kwenye utawala wa milenia. Mungu atatimiza unabii wa juma moja ili kutimiza kusudi lake kuhusiana na Israeli (Dan.9:24)

Ni wakati wa dhiki hata mataifa wasio wayahudi nao watamwamini Yesu kupitia Injili ya Ufalme itakayohubiriwa na wale wayahudi 144,000. Hawa mataifa watakaookolewa wakati wa dhiki kuu na ambao hawatakufa kwenye dhiki ndio watakajumuika kama kondoo kwenye hukumu ya Kristo kama ilivyotabiriwa kwenye Mathayo 24.

Kusudi la pili la dhiki ni Mungu kumwaga ghadhabu yake juu ya walimwengu ambao waliikataa Injili wakati wa kipindi cha kanisa la Kristo kabla ya dhiki kuanza. Wengi wakati huu watakuwa wamejisajili chini ya utawala wa Mpingakristo na kushikiri maovu yaliyokithiri na ghadabu ya Mungu atashuka kwa ajili yao ili kupatiliza maasi yatakayokuwa yakiendelea kila mahali duniani kwa wakato huo. (2 Thes.2:11-12) Kusudi la tatu la dhiki ni kufanya hukumu dhidi ya kanisa lililokengeuka ambalo litakuwa likiongozwa na Nabii wa uongo (Ufu.17:6) Ufu.17:15-18

MCHAKATO WA MAMBO KATIKA DHIKI

Baada ya kunyakuliwa kwa Kanisa, na utendaji wa Roho Mtakatifu kutoweka juu ya uso wa dunia hii, ndipo ukengefu wa kiimani na mmomonyoko wa maadili utakithiri kupindukia. Kiwango cha uasi dhidi ya mamlaka zilizoko kitapanda na kupoteza amani ya kijamii na uhuru wa kuabudu Mungu wa kweli utatoweka katika jamii. Uvunjwa wa amri za Mungu katika Biblia utakuwa ndio mtindo wa maisha ya kila siku katika jamii. Wakati huo hakuna tena Injili ya wokovu kwa kuwa aliyekuwa mtetezi wake hayupo tena duniani. (Hivi sasa yuko azuiaye)

Kutokana na mkenguko mkubwa wa kiimani na kimaadili katika dunia nzima, Shetani atatumia fursa hiyo kumtambulisha wakala wake ambaye ni Mpingakristo ambaye atajitokeza kuwa ni mpatanisha na mtatuzi wa matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kidini ambayo yatakuwa yanasumbua dunia nzima. Huyu Mpinga Kristo atavuviwa na shetani katika kufanya hata miujiza ya uongo ili kuwadanganya walimwengu ambao waliikataa Injili ya kweli wakati kanisa la kweli la Kristo lilipokuwa bado liko duniani. (2 Thes.2:9-10)

Mojawapo ya miujiza mikubwa atakayofanya huyu Mpingakristo ni kufanikisha zoezi la kusaini mkataba wa Amani kuhusu mgogoro sugu wa Mashariki ya Kati, kati ya Israeli na Waarabu. (Dan.9:27) Mojawapo ya ushawishi wake kwa Israeli ni kukamilisha hitaji la ujenzi wa Hekalu la kiyahudi na wayahudi wataanza kutoa dhabihu za wanyama kama zamani. Na pia atafanikisha zoezi la kuundwa kwa serikali moja ya ulimwengu mzima ambapo mamlaka za mataifa binafsi yatajumuishwa pamoja chini ya utawala wa mfumo wa serikali moja ya dunia.

Wakati huo atatokea mtu mwingine mwenye ushawishi mkubwa katika mambo ya uchumi na dini (Ufu.13:11-17) Kazi ya mnyama huyu kwa jina maarufu la Nabii ya uongo atakuwa mpiga debe wa Mpingani Kristo katika kuhamasisha ulimwengu kumwabudu Mpingakristo sawa na Mungu. Atafanya ushawishi mkubwa kwa njia ya kuweka mfumo mmoja wa uchumi ambapo kila raia duniani atawajibika kujisajili kwenye mfumo huo ilia pate kufanikisha mambo yake ya kiuchumi.

AWAMU YA PILI YA DHIKI

Baada ya kipindi cha miaka mitatu na nusu ndipo awamu ya pili ya dhiki itaanza kwa Mpingakristo kuvunja mkataba wa amani aliofanya Israeli na waarabu. Mkataba huo utavunjwa kwa Mpingakristo kuingia kwenye hekalu na kujitangaza kuwa yeye ndiye Mungu na wayahudi wamwabudu yeye. Hilii ndilo linaitwa chukizo la uharibifu (Dan.9:27; 2 Thes.2:3-10)

Hii awamu ya pili ya dhiki ndiyo inaitwa DHIKI KUU, (Ufu.7:14) na ndiyo inaitwa wakati wa taabu ya Yakobo (Yer.30:7) Kilele cha dhiki kuu kitafikiwa pale ambapo Mpingakristo ataongoza vita ya kuiangamiza Israeli kuanzia Yerusalemu maarufu kwa jina la VITA YA ARIMAGEDONI. Kabla ya kutimiza mkakati huo ndipo Yesu Kristo mwenyewe ataamua kurudi mara ya pili duniani na majeshi yake ya Mbinguni na kuja kumwangamiza Mpingakristo na majeshi yake na kuwatupa kwenye ziwa la moto (Ufu.19:11-21)

Kazi ya Yesu pia itakuwa ni kumkamata Shetani mwenyewe na kumfunga kwenye shimo la giza kwa kipindi cha miaka 1000 (Ufu.20:1-6); na kisha Yesu kuweka utawala wa milenia, na makao makuu yakiwa jijini Yerusalemu.

Nachukua fursa hii kuwashukuru wote mliofuatilia mada hii na kujibu kwa njia mbali mbali. Natarajia kwamba tutaendelea kuelimishana kwenye mada mpya zinazokuja mbeleni. Mbarikiwe sana.

Comments

Popular posts from this blog

IFAHAMU NGUVU YA MSALABA