IFAHAMU NGUVU YA MSALABA


Yafuatayo ni baadhi tu ya Yale ambayo Msalaba wa Yesu umeyashughulikia;

1.UMEIVUNJA NGUVU YA DHAMBI ( 1Yohana 3:8)
Yesu alidhihirishwa ili aiharibu NGUVU YA DHAMBI…Alifanya hivyo kwa “KUZIBEBA DHAMBI ZETU MWILINI MWAKE JUU YA MTI[MSALABA], ILI TUKIWA WAFU KWA MAMBO YA DHAMBI TUWE HAI KWA MAMBO YA HAKI…” (1Petro 2:24)
2.ALILIPA GHARAMA YA DHAMBI KISHERIA (2Kor 5:21)
Yeye asiyeijua dhambi [Yesu] alifanyika dhambi ili sisi tupate kufanyika HAKI YA MUNGU…Badala ya sisi kulipia gharama ya dhambi, “MSHAHARA WA DHAMBI NI MAUTI…” Yeye Yesu kama Mwanakondoo wa Mungu(Yohana 1:28,35) alichinjwa na kulipia adhabu ya dhambi zetu…Ndio maana alipokuwa Kalvari, kwa kule KUBEBA DHAMBI ZETU MWILINI MWAKE (1Petro 2:24), Mungu alimgeuzia mgongo na kumwacha, akapaza sauti na kulia, “MUNGU WANGU, MUNGU WANGU, MBONA UMENIACHA?”

3.AMETUFANYA WENYE HAKI WA MUNGU (Rumi 8:34)
Ni nani atakayewahukumu Wateule wa Mungu [sisi tulio ndani ya Yesu]? Mungu mwenyewe ndiye mwenye kuwahesabia haki, Maana Kristo Yesu alikufa, naam amefufuka na ndiye anayetuombea.
Ndiyo maana tuna ujasiri wa kumsogelea Mungu kama BABA na si HAKIMU kwetu kwa sababu ya kazi njema msalabani aliyoifanya Yesu….”TANGU SASA HAPANA HUKUMU YA DHAMBI JUU YAO WALIO KATIKA KRISTO YESU” (Rumi 8:1)

4.ALIYAPONYA MAGONJWA YETU NA UDHAIFU WETU (1Petro 2:24)
Mwenyewe alizichukua dhambi zetu mwilini mwake, ili tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki, NA KWA KUPIGWA KWAKE MLIPONYWA!
Biblia haisemi mnaponywa, inasema “MLIPONYWA” Ilifanyika pale msalabani tayari, sio kitu tunachokitafuta sasa au kesho…Msalaba ulioshughulikia DHAMBI ni huo huo uliokomesha Magonjwa yote na madhaifu yetu…UKIWA MGONJWA UMETAKA MWENYEWE, na wala usimsumbue Mungu kwamba akuponye…ALIFANYA HILO MIAKA ZAIDI YA MIAKA 2000 ILIYOPITA, Ndani ya kitabu changu “SABABU SABA ZA KIBIBLIA KWANINI USIWE MGONJWA” Nimelizungumzia hili kwa upana zaidi, JIPATIE NAKALA YAKO!
5.ALISHUGHULIKIA AMANI YETU (Isaya 53:5)
…Na adhabu ya AMANI YETU ilikuwa juu yake!
Kabla ya Kwenda msalabani, Yesu alitoa ahadi ya kutupatia AMANI YAKE, na akasema atupavyo Yeye ni tofauti na ulimwengu utoavyo
 (Yohana 14:27) na huo ulikuwa ni mkataba usiopitishwa, ulikuwa MSWADA wa kile ambacho alitaka kutupatia…alipokwenda Msalabani, alikamilisha hilo, sawa na nabii Isaya alivyotabiri zaidi ya miaka 600 kabla ya kifo chake!

6.ALIKOMESHA HUZUNI NA MASIKITIKO KWA KILA ALIYE WA KWAKE (Isaya 53:4)
Hakika ameyachukua MASIKITIKO YETU, amejitwisha HUZUNI ZETU!
Ndio maana tangu Kristo akishinde kifo na mauti, mahali pote ROHO MTAKATIFU kupitia kinywa cha Mtume Paulo aliwaambia Wafilipi, “FURAHINI KATIKA BWANA, TENA NASEMA FURAHINI, UPOLE WENU NA UJULIKANE NA WATU WOTE, BWANA YU KARIBU”
 (Wafilipi 4:4)

Hakuishia hapo, bali alizungumza tena na kanisa la Thesalonike akisema, “FURAHINI SIKU ZOTE. OMBENI BILA KUKOMA, SHUKURUNI KWA KILA JAMBO, MAANA HAYA NDIYO MAPENZI YA MUNGU KATIKA KRISTO YESU”
 (1Wathesalonike 5:16-18)
Ndio maana alipotupatia ROHO MTAKATIFU, kati ya MATUNDA anayoyatoa ni FURAHA (Wagalatia 5:22) kwa sababu alijua pasipo UWEZESHO NA NGUVU YA MUNGU MWENYEWE, tutapitia changamoto ambazo zitatuzuia kufurahi siku zote na nyakati zote, akamtoa MSAIDIZI-ROHO MTAKATIFU aje na package ya FURAHA pia kama kati ya MATUNDA YAKE!.

MUNGU WA MBINGUNI AKUBARIKI.

Comments

Popular posts from this blog